Habari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zinaeleza kuwa Rais Félix Antoine Tshisekedi huenda ameanza kumwandaa mwanawe, Anthony Tshisekedi, ili awe mrithi wake katika uongozi wa nchi.
Kwa sasa, Anthony hana nafasi rasmi katika serikali ya DRC.
Hata hivyo, tangu mwaka 2021, amekuwa akisafiri na Rais Tshisekedi kwenye ziara mbalimbali za kimataifa, ingawa ziara hizo zimekuwa zikifanywa kwa usiri mkubwa.
Mojawapo ya matukio machache ambayo Anthony alionekana hadharani kama sehemu ya ujumbe wa serikali ya DRC ni wiki iliyopita alipohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Ghana, John Mahama Dramani.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Rais Félix Antoine Tshisekedi pamoja na mkewe, Denise Nyakeru Tshisekedi.
Moja ya picha zilizopigwa kwenye hafla ya kuapishwa kwa John Dramani inaonyesha Anthony Tshisekedi akiwa karibu na Rais Paul Kagame wa Rwanda. Picha hiyo imezua gumzo kubwa miongoni mwa raia wa Kongo, wakijiuliza ni nafasi gani kijana huyo anayo inayomruhusu kuhudhuria hafla ya kiwango hicho.
Tetesi ziliongezeka zaidi Ijumaa iliyopita wakati Anthony alipohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais Nicolás Maduro wa Venezuela kama sehemu ya ujumbe ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Seneti ya Kongo, José Kalala wa Kalala.
Awali, ilitarajiwa kuwa Rais Tshisekedi angehudhuria hafla hiyo, lakini aliamua kurejea DRC ambapo aliendesha mkutano wa Baraza Kuu la Kijeshi mwishoni mwa juma.
Wakati huohuo, picha zilizoenea mtandaoni zinaonyesha Anthony Tshisekedi akikutana na Rais Maduro katika Ikulu ya Venezuela.
Ripoti kutoka DRC zinaeleza kuwa Rais Félix Antoine Tshisekedi ameamua kumtambulisha mwanawe kwenye uwanja wa siasa, ili aweze kumrithi endapo juhudi zake za kubadilisha katiba zitashindikana.
Kwa sasa, Tshisekedi anapambana kubadilisha katiba ili aweze kugombea muhula wa tatu, lakini anakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa wanasiasa kama Joseph Kabila, Moïse Katumbi na Martin Fayulu.
Inasemekana kuwa mpango wa kumwandaa Anthony ni mbadala ikiwa juhudi za kubadilisha katiba zitashindikana.
Hata hivyo, mwandishi wa habari Baelenge Irenge anaripoti kuwa Denise Tshisekedi, mke wa rais, hapendezwi na wazo la Anthony kurithi madaraka, kwani si mwanawe wa kumzaa.
Anthony Tshisekedi akiwa karibu na Rais Kagame wakati wa sherehe za Ghana
Anthony Tshisekedi akikutana na Rais Maduro wa Venezuela.


