Rwanda imewaruhusu wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliotumwa mkoani Kivu Kaskazini, DRC, kupambana na waasi wa M23, kupita katika ardhi yake wakielekea makwao.
Wanajeshi hao waliwasili Desemba 2023 kusaidia jeshi la serikali ya DRC katika mapambano dhidi ya waasi wa M23.
Tangu mwisho wa Januari 2025, wanajeshi hao waliokuwa chini ya ujumbe wa SAMIDRC wamekwama mjini Goma na Mubambiro, baada ya vikosi vya serikali kushindwa vibaya na M23.
M23 hivi karibuni waliwataka wanajeshi wa SADC kuondoka mara moja Goma, wakidai walihusika kwenye mashambulizi ya tarehe 11 Aprili 2025 yaliyoendeshwa na majeshi ya serikali ya Kinshasa.
Hii ilitokea wakati SADC tayari ilikuwa imesitisha rasmi operesheni yake katika eneo hilo.
Kwa kuwa njia ya anga haiwezekani kutokana na uharibifu wa uwanja wa ndege wa Goma, wanajeshi hao wanatarajiwa kupita kwa barabara kupitia Rwanda.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, mazungumzo kati ya SADC na Serikali ya Rwanda yalikuwa yanaendelea kwa siku kadhaa, na sasa Rwanda imekubali kutoa njia hiyo, kulingana na wanadiplomasia watatu waliozungumza na shirika la habari la Reuters.
Vyanzo viwili vya ziada vilisema silaha za wanajeshi hao zitazuiwa kwa muda wakiwa ndani ya Rwanda kwa sababu za kiusalama, na zitarudishwa tu baada ya kuondoka nchini humo.


