Mahakama Kuu ya Rwanda imeahirisha kesi ya Vincent Murekezi, anayeshutumiwa kwa makosa ya kuhusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi, baada ya kuomba muda zaidi kutafuta wakili mpya. Wakili wake wa awali alijiondoa kwenye kesi hiyo bila kumjulisha.
Kesi hiyo ilifanyika Alhamisi hii kwa njia ya video kutoka gereza la Mageragere jijini Kigali. Murekezi aliieleza mahakama kuwa ana ugumu wa kuwasiliana na familia yake inayoishi nje ya Rwanda ili wamsaidie kupata wakili mpya. Alisisitiza kuwa hawezi kujitetea bila msaada wa wakili.
Mahakama ilikubali kumsaidia kuwasiliana na familia yake kadri iwezekanavyo, na ikaahirisha kesi hadi mwezi wa tisa ili kumpa muda wa kujipanga na kupata wakili mpya.
Mwaka 2019, Murekezi alirudishwa kutoka Malawi kuja Rwanda kufunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya kimbari yaliyotokea katika mji wa zamani wa Butare, sasa ukiwa wilaya ya Huye.
Alikata rufaa dhidi ya kifungo cha maisha alichohukumiwa na Mahakama ya Kati ya Huye, ambayo ilimpata na hatia kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari. Hata hivyo, Murekezi amekana mashtaka hayo vikali.
Mahakama za Gacaca mjini Butare, anakotoka, na Mahakama ya Kati ya Huye zilimhukumu kifungo cha maisha jela kwa kushiriki moja kwa moja katika mauaji hayo wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.
Murekezi, mwenye umri wa miaka 62, anaripotiwa kuwa alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini Malawi. Alirudishwa Rwanda kupitia makubaliano ya kisheria kati ya Malawi na Rwanda ya kubadilishana washukiwa wa uhalifu.
Mamlaka za haki nchini Rwanda zinasema alirudishwa Rwanda pia ili amalizie kifungo cha miaka minne kwa kosa la rushwa alichohukumiwa nchini Malawi, ambapo alibakiwa na miaka miwili, sambamba na kesi ya mauaji ya kimbari.
Mwendesha mashtaka anasema Murekezi alikuwa miongoni mwa viongozi wa mauaji katika mji wa Butare, akitoa maagizo kwenye vizuizi mbalimbali ambako Watutsi wengi waliuawa.


