Jumapili tarehe 8 Juni 2025, timu ya taifa ya Ureno iliandika historia tena kwa kutwaa taji lao la pili la UEFA Nations League baada ya kuifunga Uhispania kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia sare ya 2-2. Ushindi huo ulimwachia Cristiano Ronaldo machozi ya furaha, akionyesha hisia na matunda ya miaka mingi kama nahodha wa taifa.
Mechi hiyo ilifanyika katika uwanja wa Allianz Arena nchini Ujerumani, na ilikuwa ya kusisimua na yenye mabadiliko mengi. Uhispania walifungua ukurasa wa magoli dakika ya 21 kupitia MartÃn Zubimendi, lakini Ureno walisawazisha dakika tano baadaye kupitia kwa Nuno Mendes.
Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, Mikel Oyarzabal aliipatia Uhispania goli la pili, na wakaenda mapumziko wakiwa mbele kwa 2-1.
Cristiano Ronaldo, nahodha mwenye umri wa miaka 40, aliokoa Ureno dakika ya 61 kwa kufunga bao la kusawazisha – bao lake la 138 akiwa na timu ya taifa. Alibadilishwa kabla ya muda wa nyongeza kuanza.
Nuno Mendes, aliyefunga bao na pia kucheza vizuri upande wa ulinzi, alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi. Alikuwa na mchango mkubwa kwa ushindi wa Ureno na alimzuia kikamilifu kijana wa Uhispania, Lamine Yamal, kuonesha makali yake.
Ureno imekuwa timu ya kwanza katika historia ya mashindano haya kushinda UEFA Nations League mara mbili, baada ya ushindi wao wa kwanza mwaka 2019. Kwa upande mwingine, Uhispania imeshindwa kurejesha taji ililotwaa mwaka 2023.


