Jumapili hii, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeonyesha wasiwasi wake mkubwa kuhusu kile inachokiona kama mwelekeo wa hatari: “kujiondoa kwenye makubaliano au kuvuruga mazungumzo pale ambapo uwajibikaji unahitajika.” DRC pia imelituhumu Rwanda kwa kukivunja Kifungu cha 34 cha mkataba wa ECCAS, kufuatia hatua ya kuzuia uongozi wa Rwanda ndani ya jumuia hiyo.
Kinshasa inaamini kwamba tabia hii, ambayo inasema “imevumiliwa kwa muda mrefu,” imesababisha “makubaliano kutotekelezwa, hivyo kupoteza maana.” Serikali ya Congo ilitoa tamko hilo baada ya Rwanda kujiondoa kwenye Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS).
DRC ilisisitiza kuwa mzozo wake na Rwanda umezidi kuwa mbaya kwa sababu ya vitendo vya uchokozi, ambavyo vimekataliwa vikali kupitia azimio la 2773 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linalotaka wanajeshi wa Rwanda kuondoka mara moja kwenye ardhi ya Congo. Kinshasa inasema vitendo hivyo vinakiuka moja kwa moja Kifungu cha 34 cha mkataba ulioboreshwa wa ECCAS, ambacho kinakataza matumizi ya nguvu kati ya nchi wanachama.
“Sheria lazima itekelezwe kikamilifu au inakosa maana kabisa,” ilisema Kinshasa, ikisisitiza kuwa inaendelea kuunga mkono juhudi za kutafuta amani zinazoongozwa na Umoja wa Afrika, Qatar na Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya DRC ilisisitiza:
“Kushiriki kwenye mchakato wa amani hakumaanishi kusahau yaliyopita au kutoa kinga kwa makosa makubwa.”
Ilitoa wito kwa mamlaka za kanda na kimataifa kuhakikisha “wanathibitisha kwa vitendo dhamira yao ya kuheshimu sheria, majukumu na uhuru wa nchi.”


