Niyongabo Jules, mmoja wa wagombea waliowania nafasi katika Bunge la Burundi, amelaani jinsi uchaguzi wa hivi karibuni ulivyofanyika, akisema kuwa kulikuwa na wizi wa kura.
Alitoa kauli hiyo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa bunge uliofanyika Juni 5, ambapo ilibainika kuwa chama tawala cha CNDD-FDD kilishinda kwa asilimia 100.
Hii ina maana kwamba chama cha CNDD-FDD kitakuwa chama pekee bungeni, pamoja na wawakilishi watatu kutoka jamii ya Batwa.
Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano, tarehe 11 Juni, baada ya kutangazwa kwa matokeo na Tume Huru ya Uchaguzi, Niyongabo alisema kuwa hata kura yake aliyojipigia iliibwa na kupewa CNDD-FDD.
Alisema:
“Tulijua kuwa Burundi ina matatizo fulani, lakini sasa tumeona kuwa kuna matatizo mengine makubwa zaidi ambayo yatahitaji nguvu kubwa ili Waburundi wajikomboe kutoka katika hali hii ambapo uchaguzi unafanyika, lakini mtu anakuta kura yake haipo. Mimi nilipopiga kura, nilikuta hakuna kitu — hata kura yangu haikuwepo.”
Niyongabo alisema kwamba kama Waburundi wengine wengi, aliumizwa sana na jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika.
Aliongeza kuwa alishangazwa kuona kwamba kura zote zilikwenda kwa CNDD-FDD, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Burundi.
Alisema:
“Wakati wa Ndadaye, Waburundi walikuwa wamechoka zaidi kuliko sasa, lakini hakuwahi kupata zaidi ya asilimia 60, wala 70%. Hata Rwagasore, aliyekuwa akitusaidia katika harakati za uhuru, hakuwahi kufikia 70%.”
Aliendelea:
“Nyakati zile zilikuwa ngumu sana kuliko sasa, lakini bado watu hawakumpa asilimia 80 au 90 kama inavyodaiwa sasa.”
Vyama vya upinzani kama UPRONA na CNL pia vimekataa matokeo ya uchaguzi huo.
Wakati wa uchaguzi, baadhi ya raia walisema walipelekwa kwenye chumba cha kupigia kura wakiwa wamelazimishwa kupigia kura chama tawala.
Wengine walidai walipofika kupiga kura walikuta kura tayari zimepigwa kwa niaba yao.


