Ripoti zinaonyesha kuwa takriban majenerali 20 wa ngazi za juu wa jeshi la Iran waliuawa na Israel katika mashambulizi ya anga siku ya Ijumaa iliyopita.
Mashambulizi hayo yalifanywa na ndege za kivita zipatazo 200 kutoka Israel, zikiwemo ndege za kisasa aina ya F-35.
Iran imethibitisha kuwa angalau makamanda wake watatu wa juu walikuwa miongoni mwa waliouawa.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alitangaza Ijumaa kuwa watu 78 waliuawa katika mashambulizi hayo ya Israel, ambayo Israel inadai yalilengwa kufyekelea vituo vya uzalishaji wa silaha za nyuklia. Zaidi ya watu 320 walijeruhiwa.
Miongoni mwa waliouawa walikuwemo maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu, wataalamu mashuhuri wa kisayansi, na wanasiasa wakuu.
Aliyekuwa mkuu wa jeshi la nchi kavu Meja Jenerali Mohammad Bagheri, ambaye pia alikuwa mtu wa pili kwa nguvu katika jeshi la Iran baada ya Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, alikuwa miongoni mwa waliouawa.
Bagheri alichukuliwa nafasi yake na Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi siku hiyo hiyo.
Mwingine aliyeuawa alikuwa Jenerali Hossein Salami, aliyekuwa kiongozi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) — jeshi kuu la Iran. Alichukuliwa nafasi yake na Jenerali Mohammad Pakpour.
Wa tatu ni Jenerali Gholamali Rashid, ambaye alikuwa Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Iran.
Wengine waliouawa ni:
-
Jenerali Amir Ali Hajizadeh, mkuu wa Jeshi la Anga la Iran
-
Gholamali Rashid, kiongozi wa Makao Makuu ya Khatam-al Anbiya, kitovu cha operesheni za kijeshi cha Iran
Mbali na majenerali hao, Iran ilimpoteza pia Ali Shamkhani, mwanasiasa aliyekuwa na uaminifu mkubwa kwa Ayatollah Khamenei, ambaye alikuwa kiongozi wa mazungumzo ya kuacha uzalishaji wa silaha za nyuklia kati ya Iran na Marekani.
Wataalamu waliouawa ni pamoja na:
-
Fereydoon Abbasi, aliyekuwa mkuu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran (2011–2013), na mbunge kati ya 2020–2024
-
Mohammad Mehdi Tehranchi, rais wa Chuo Kikuu cha Azad mjini Tehran
-
Abdulhamid Minouchehr, kiongozi wa utafiti wa silaha za nyuklia katika Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti
-
Ahmad Reza Zolfaghari, mhadhiri wa teknolojia ya silaha za nyuklia katika chuo hicho
-
Amirhossein Feqhi, ambaye pia alikuwa mtafiti wa aina hiyo katika taasisi hiyo


