Tarehe 13 Juni, siku ya Ijumaa, Rwanda ilikabidhiwa rasmi uongozi wa Jumuiya ya Kudhibiti Usambazaji Haramu wa Silaha Ndogo Afrika (RECSA).
Majukumu haya yalipitishwa katika mkutano wa 11 wa mawaziri wa nchi wanachama wa RECSA, uliofanyika Nairobi, Kenya.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Rwanda, Dkt. Vincent Biruta, alipokea bendera na vifaa rasmi vya RECSA kutoka kwa mwenzake wa Kenya, Kipchumba Murkomen.
Rwanda linachukua uongozi kutoka kwa Kenya, huku Tanzania ikitarajiwa kusaidia kama msaidizi wa uongozi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Olivier Nduhungirehe, alifichua kuwa kabla ya Rwanda kupewa uongozi huo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilijaribu kuzuia uteuzi wa Rwanda, lakini ikashindwa.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa X alisema:
“Ni muhimu kufahamu kuwa DRC ilijaribu tena kupinga Rwanda kuongoza RECSA. Kwa bahati nzuri, mashirika ya Kiafrika hayawezi kuogopeshwa wala kutumika kama vyombo na serikali ya Kinshasa iliyojaa kukata tamaa.”
Hii siyo mara ya kwanza kwa DRC kujaribu kumzuia Rwanda. Wiki iliyopita, ilifanikiwa kuzuia Rwanda kuchukua uongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS), ingawa Rwanda ndiyo ilikuwa inastahili kuchukua nafasi hiyo.
Hatua hiyo iliwaudhi sana viongozi wa Kigali, ambao walichukua uamuzi wa kujiondoa kwenye CEEAC, wakishutumu kuwa jumuiya hiyo inatumika kisiasa na DRC kwa msaada wa baadhi ya wanachama.


