Majira ya saa sita mchana Jumamosi hii, ajali mbaya imetokea jijini Kigali, katika eneo la stendi ya mabasi ya Nyabugogo.
Gari la abiria, linaloaminika kuwa linafanya safari ndani ya Kigali, liligonga jengo ambalo hutumika kwa kuuza tiketi za usafiri za kampuni ya Zebra.
Mashuhuda wamesema kuwa gari hilo lilikosa breki, kisha likawagonga watu na likabomoa ukuta wa jengo, ambao uliangukia baadhi ya watu waliokuwa ndani.
Polisi wa Rwanda, kupitia ukurasa wao wa X, walisema kuwa walifika haraka eneo la tukio na kuanza uchunguzi wa chanzo cha ajali.
Ingawa idadi rasmi ya majeruhi au waliokufa haijatolewa, waliokuwepo eneo hilo wanasema kuwa watu kadhaa walipoteza maisha.
Magari ya wagonjwa yalifika mapema na kuwahamisha majeruhi kwenda hospitalini.
Polisi wanaendelea kufuatilia tukio hilo kwa undani ili kubaini ukweli kamili.


