Victoire Ingabire Umuhoza anatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama ya Mwanzo ya Kicukiro siku ya Jumanne, Julai 8, 2025, katika kesi ya ombi la kuachiliwa kwa muda, kwa mujibu wa The New Times.
Kesi hiyo inafuatia kukamatwa kwake mnamo Juni 19, 2025, kwa tuhuma za kusambaza habari za uongo na uvumi unaolenga kuharibu sura ya Rwanda kimataifa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPPA), Ingabire — aliyewahi kufungwa kwa makosa ya uchochezi na kuunda makundi ya kijeshi — sasa anatuhumiwa kwa kuhatarisha tena usalama wa umma.
Kesi yake iliwasilishwa mahakamani mnamo Juni 30, baada ya uchunguzi kufanywa na Ofisi ya Upelelezi ya Rwanda (RIB).
Ingabire ni kiongozi wa chama cha siasa DALFA-Umurinzi, ambacho hakijatambuliwa kisheria. Alihukumiwa miaka 15 gerezani kwa makosa ya uchochezi dhidi ya serikali, kuunda kundi la waasi, na kupuuza mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994. Aliachiwa huru mwaka 2018 kwa msamaha wa Rais Paul Kagame.
Mashtaka yanasema kuwa kesi yake imeunganishwa na ya YouTuber Theoneste Nsengimana na Sylvain Sibomana, wanaoshutumiwa kwa kuandaa mafunzo ya maandamano ya amani kupitia masomo ya Kiingereza, wakitumia kitabu Blueprint for Revolution cha Mserbia Srdja Popovic.
Washitakiwa wote wanadaiwa kutekeleza mipango yao kwa siri, wakitumia majina ya uongo, na kutafuta msaada wa kifedha kutoka nje ya nchi.
Mahakama itaamua kama washtakiwa waendelee kushikiliwa rumande wakati uchunguzi ukiendelea.


