Ripoti kutoka kwa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zinaonyesha kuwa serikali ya Kinshasa imeandaa karibu wanajeshi 60,000 kwa ajili ya kuchukua tena miji ya Goma na Bukavu, ambayo imekuwa chini ya udhibiti wa waasi wa M23 kwa karibu miezi sita.
Hii inajiri siku chache tu baada ya DRC kusaini makubaliano ya amani na Rwanda, huku ikiendelea kupeleka jeshi kutoka Burundi pamoja na silaha nzito.
Muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC) unaojumuisha M23 umelaani vikali hatua hiyo, ukisema ni kampeni ya ghasia inayo hatarisha maisha ya raia.
Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, alisema kuwa kuendelea kwa urundikaji wa wanajeshi ni dhihaka kwa mazungumzo ya amani yanayoendelea kati ya pande hizo.
Aliongeza, “Kitu kibaya zaidi ni kwamba jeshi la Burundi linatoa silaha nzito kuelekea maeneo yenye wakazi wengi. Hili ni jinai dhidi ya ubinadamu.”
Ingawa serikali ya DRC haijatangaza rasmi idadi ya wanajeshi waliotumwa, duru za kijeshi zinasema huu ndio mpango mkubwa zaidi wa kijeshi tangu mwaka 2013, wakati jeshi la DRC lilishirikiana na MONUSCO dhidi ya M23.
Maafisa wa serikali wanasema maandalizi haya ni muhimu kwa ajili ya kudhibiti tena Goma, Bukavu, na maeneo mengine yanayoshikiliwa na M23 tangu mwisho wa 2021.
Hali ya taharuki imeongezeka, hasa baada ya wiki moja tu tangu kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda, ambayo pia yalihusisha mazungumzo ya haraka na M23.
Hata hivyo, kutoaminiana kati ya pande hizo kunatia shaka utekelezaji wa makubaliano hayo.
Rais Paul Kagame alisema Rwanda iko tayari kutekeleza makubaliano hayo, lakini akaonya kuwa ikiwa upande wa pili utakuja na ujanja au kuchelewesha suluhisho, “tutamaliza tatizo kama zamani.”
Akamalizia kwa kusema: “Sisi tuna mpango, tuna ukweli, na tumeazimia kutekeleza makubaliano kwa ukamilifu ili kumaliza mgogoro huu.”


