Afisa mwandamizi wa kijeshi wa Hamas ameiambia BBC kwamba kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina limepoteza karibu asilimia 80 ya Ukanda wa Gaza, huku familia za wenye silaha zikijaza pengo la uongozi.
Lieutenant Colonel huyo, ambaye alijeruhiwa wiki ya kwanza ya vita vilivyoanza tarehe 7 Oktoba 2023 baada ya Hamas kushambulia Israel, amesema kuwa miundo ya kijeshi, kisiasa na kiusalama ya Hamas imeporomoka kutokana na miezi ya mashambulizi ya Israel.
Kutokana na hali yake ya kiafya, sasa hayupo tena kazini, lakini alituma jumbe kadhaa za sauti kwa BBC, akiomba jina lake lisitajwe.
Katika sauti hizo, alieleza kuhusu kuvunjika kwa Hamas kutoka ndani, pamoja na kuporomoka kwa usalama katika Gaza, eneo ambalo walikuwa wakilidhibiti kabla ya mgogoro.
“Tuwe wa kweli—hakuna kilichosalia katika mfumo wetu wa usalama. Asilimia 95 ya viongozi wetu wameuawa, na wapiganaji wengi wamekufa. Kwa hivyo, ni nini kinachoweza kuizuia Israel kuendelea na vita hivi?”
Akaongeza:
“Kimaantiki, lazima waendelee hadi mwisho. Israel ina nguvu ya kijeshi, dunia inanyamaza, serikali za Kiarabu hazisemi chochote, makundi ya wahalifu yako kila mahali, na jamii inaporomoka.”
Mwezi Septemba mwaka jana, Waziri wa Ulinzi wa Israel alisema kuwa “Hamas kama jeshi halipo tena”, na kuwa sasa limegeuka kuwa vuguvugu la msituni.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, Hamas ilijaribu kujiimarisha tena wakati wa siku 57 za usitishaji vita mapema mwaka huu kwa kuimarisha muundo wa kisiasa, kijeshi na kiusalama.
Hata hivyo, baada ya Israel kuvunja mkataba wa usitishaji vita mwezi Machi, walishambulia viongozi waliokuwa wamebaki, jambo lililosababisha Hamas kuporomoka kabisa.


