Hivi karibuni, Afrika Kusini ilituma wanajeshi wa ziada na vifaa vya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kupoteza wanajeshi 14 huko.
Habari hii ilithibitishwa na shirika la habari la Uingereza, Reuters, kupitia vyanzo vya kidiplomasia na kisiasa.
Afrika Kusini imetuma wanajeshi wa ziada huku kukiwa na hofu kwamba vita vinavyoendelea mashariki mwa Kongo vinaweza kuongezeka zaidi.
Rekodi za safari za ndege zinaonyesha kuwa ndege imekuwa ikifanya safari kati ya Afrika Kusini na Lubumbashi kwa siku kadhaa.
Mbunge mmoja wa Afrika Kusini aliliambia Reuters kuwa kati ya wanajeshi 700 na 800 wa Afrika Kusini tayari wamewasili Lubumbashi.
Mbunge Chris Hattingh alisema: “Tumejulishwa kuwa wanajeshi wamekusanyika Lubumbashi. Tumepata taarifa kwamba wanajeshi kati ya 700 na 800 wako Lubumbashi.”
Mbunge huyu, ambaye pia ni msemaji wa muungano wa chama tawala cha Democratic Alliance, aliongeza kuwa ni vigumu kujua kinachoendelea kwa sababu Kamati ya Bunge ya Ulinzi haikujulishwa kuhusu kupelekwa kwa wanajeshi hawa.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Afrika Kusini alithibitisha kuwa anafahamu juu ya wanajeshi waliotumwa Lubumbashi, lakini alikataa kutoa maelezo zaidi.
Ripoti zinaonyesha kuwa Afrika Kusini ina wanajeshi wapatao 3,000 katika DRC, wakiwemo wale walio katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani (MONUSCO) pamoja na wale walio chini ya ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SAMIDRC).
Nchi hiyo inazidisha uwepo wake wa kijeshi katika Kongo wakati ambapo serikali yake inakabiliwa na shinikizo la kuwaondoa wanajeshi wake kutoka mashariki mwa Kongo, kwa kuwa Afrika Kusini haina maslahi ya moja kwa moja katika vita vinavyoendelea huko.


