Kamanda Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametangaza kuwa mtoto wake wa kwanza, Ruhamya Kainerugaba, amejiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), kufuata nyayo za baba yake.
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Muhoozi alieleza kuwa baada ya kujiunga na UPDF, Ruhamya alipokea cheo cha Private, ambacho ni cheo cha chini kabisa jeshini.
Akaandika:
“Nina furaha kubwa kutangaza kwamba baada ya miaka 31 nikihudumu katika Jeshi la Mungu, UPDF, Mungu ameibariki familia ya Museveni kwa kumpa askari mwingine kuanzia mwezi uliopita. Private Ruhamya Kainerugaba. Mungu ambariki kama alivyonibariki mimi.”
Ruhamya Kainerugaba mwenye umri wa miaka 24, ni mtoto wa kwanza wa Jenerali Muhoozi na mkewe Charlotte Kainerugaba.
Amejiunga na jeshi kufuata nyayo za baba yake, pamoja na babu zake: Rais Yoweri Kaguta Museveni na kaka yake Rais, Jenerali Salim Saleh.


