Jumamosi tarehe 17 Mei, Rwanda ilipokea zaidi ya watu 360 waliokuwa wakishikiliwa kama mateka na kundi la waasi wa FDLR katika misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Watu hao waliingia Rwanda wakitokea Goma na walipokelewa katika Wilaya ya Rubavu siku ya Jumamosi.

Wengi wa waliopokelewa ni wanawake, pamoja na watoto wadogo sana waliozaliwa katika misitu ya Kongo.
Walifunguliwa huru kufuatia mapigano ya mwezi Januari mwaka huu, ambapo kundi la waasi wa M23 walichukua maeneo kadhaa, yakiwemo Jiji la Goma, baada ya kuwashinda wanajeshi wa serikali ya DRC walioungana na FDLR.
Baada ya kuwasili Rwanda, wanatarajiwa kuhamishiwa katika kituo cha Mutobo kilichoko Wilaya ya Musanze, ambako watasaidiwa kuanza maisha ya kawaida kabla ya kuunganishwa tena na familia zao.
Mkuu wa Wilaya ya Rubavu, Mulindwa Prosper, aliambia waandishi wa habari kwamba watu hao ni miongoni mwa zaidi ya 2,000 wanaotarajiwa kupokelewa katika siku zijazo.


