Huzuni na simanzi vimekumba jamii ya wanafunzi wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Université du Québec à Chicoutimi (UQAC), baada ya mwanafunzi kutoka Burundi mwenye umri wa kati ya miaka 20 na 25 kujiua baada ya kushindwa mitihani.
Marafiki zake wanasema alikuwa na huzuni kali kutokana na kushindwa kwake katika masomo, huku akihisi presha kubwa kutoka kwa familia yake iliyomfadhili kwa matumaini makubwa ya kufanikisha ndoto ya masomo ya nje ya nchi.
Sadou Diallo, Rais wa MAGE-UQAC, alisema:
“Kujiua kwake ni kielelezo kwamba wengi wanateseka kimya kimya, wakihofia kuomba msaada kutokana na tamaduni zao zinazokataza kuzungumzia afya ya akili.”
Mwanafunzi huyo alikuwa amesoma UQAC kwa miaka miwili, akiwa na ndoto ya kuhitimu na kusaidia familia yake. Hata hivyo, watu wa karibu walisema kuwa kushindwa kwake, aibu, na hofu ya kufeli kulimpeleka kwenye msongo mkubwa wa akili hadi kuamua kujiua.
Hermann Kouadjo, Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kimataifa (AEI), alisema:
“Katika tamaduni zetu za Kiafrika, kujiua ni mwiko. Huonekana kama aibu, na hufanyika kwa siri. Hapa Canada kuna njia nyingi za msaada, lakini wanafunzi wengi hawajazikubali bado.”
Ripoti ya Alliance pour la santé étudiante au Québec inaonyesha kuongezeka kwa wanafunzi wanaotafuta msaada wa afya ya akili kwa mwaka wa masomo 2024–2025. Hata hivyo, viongozi wa wanafunzi wanasema wengi wanaogopa athari kwa hadhi yao ya uhamiaji.
Mnamo Novemba 2023, mwanafunzi mwingine kutoka Guinea, Mamadou Salinou Baldé, aliuawa na polisi mjini Chicoutimi baada ya kujaribu kuwashambulia akiwa na silaha. Marafiki zake walidai alikuwa na matatizo makubwa ya akili, hata kama ripoti ya coroner haikufafanua chanzo halisi.
Uongozi wa UQAC umesema kuwa umeanzisha msaada wa saa 24 kupitia jukwaa la Dialogue, pamoja na huduma bora za ushauri.
Mwezi Agosti, chuo kitazindua mpango maalum wa kuhamasisha wanafunzi kuhusu afya ya akili, kuzuia msongo, kushughulikia upweke, na kujenga mshikamano kati yao.


