Mazungumzo ya muda mrefu kati ya kundi la waasi la M23 na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yamesitishwa rasmi kufuatia kutokubaliana kwa pande zote mbili.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu, pande hizo mbili zilikuwa zikikutana kutafuta suluhu ya mzozo uliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Mazungumzo haya yaliandaliwa na utawala wa kifalme wa Qatar, ambao hapo awali uliwakutanisha Rais Félix Antoine Tshisekedi wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda jijini Doha.
Wajumbe kutoka pande zote mbili walikaa jijini Doha kwa wiki tatu kabla ya kuondoka masaa machache yaliyopita.
Mpaka sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu mazungumzo au makubaliano yoyote yaliyofikiwa.
Kwa mujibu wa Jeune Afrique, mazungumzo haya hayakuzaa matunda kutokana na mvutano mkali uliokuwepo.
Miongoni mwa masuala yenye utata, ni suala la kuachiliwa kwa wanachama wa M23 walioko kizuizini chini ya serikali ya Kinshasa.
Hivi karibuni, Kinshasa iliachia wafungwa watano baada ya M23 kuondoa wanajeshi wake Walikale, lakini kundi hilo la waasi lilikataa hatua hiyo, likisema kuwa walioachiliwa hawamo kwenye orodha yao rasmi ya wafungwa.
Kwa sasa, M23 imewasilisha Qatar orodha ya watu wapatao 700 wakiwemo wanajeshi na wanasiasa, wanaodaiwa kushikiliwa kinyume cha sheria na serikali ya Kinshasa.
Wengine waliomo kwenye orodha hiyo ni waliokamatwa kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na Christophe Baseane Nangaa, aliyekuwa Gavana wa Jimbo la Haut-Uelé na kaka yake Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa Alliance Fleuve Congo unaounga mkono M23.


