Serikali ya Burkina Faso imetangaza kuwa imefanikiwa kuzima njama ya mapinduzi iliyolenga kumuondoa madarakani Kapteni Ibrahim Traoré. Mamlaka zinasema njama hiyo ilipangwa na watu walioko nchini Côte d’Ivoire.
Jumanne, Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, alisema jaribio hilo lilihusisha wanajeshi waliopo kazini na wengine wa zamani waliotuhumiwa kushirikiana na viongozi wa makundi yenye msimamo mkali.
Alifafanua kuwa walipanga kuvamia makazi ya rais na kusababisha machafuko ambayo yangetoa mwanya kwa mataifa ya kigeni kuingilia uongozi wa nchi hiyo.
Sana aliongeza kuwa njama hiyo pia ilihusisha ushirikiano na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel kwa lengo la kuongeza mashambulizi dhidi ya jeshi na raia.
Kapteni Ibrahim Traoré ameiongoza Burkina Faso tangu 2022 baada ya kuchukua madaraka kupitia mapinduzi. Kwa kipindi cha miaka mitatu, tayari jaribio kadhaa ya kumuondoa madarakani yameripotiwa, ikiwemo moja Novemba mwaka jana.
Serikali imethibitisha kuwa jaribio hili la hivi karibuni lilizimwa wiki iliyopita, na wanajeshi kadhaa akiwemo maafisa wawili wakuu kukamatwa kwa kuhusika.


