Kikundi cha waasi cha M23 na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wametangaza matokeo ya mazungumzo ya ana kwa ana yaliyofanyika Qatar.
Pande hizo mbili zilikuwa kwenye majadiliano kwa takriban wiki tatu, chini ya usimamizi wa ufalme wa Qatar, kwa lengo la kutafuta suluhisho la mzozo uliodumu tangu Novemba 2021.
Kupitia taarifa iliyotiwa saini na Papy Mbuyi Kanguvu, kiongozi wa ujumbe wa serikali ya DRC, serikali ilieleza kuwa mazungumzo yalikuwa “ya amani na yenye mafanikio.” M23 pia ilitoa taarifa kama hiyo iliyosainiwa na msemaji wake wa kisiasa, Lawrence Kanyuka.
Pande zote mbili zilikubaliana kuwa kuna maeneo ambayo walifikia mwafaka, licha ya taarifa zilizokuwa zikidai kuwa mazungumzo yalikuwa yamesimama baada ya serikali ya DRC kukataa kuwaachilia zaidi ya watu 700 waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika na M23.
Miongoni mwa makubaliano yaliyotangazwa ni:
-
Kusitisha mapigano mara moja
-
Kukomesha hotuba za chuki na vitisho
-
Wito kwa makabila yote ya Congo kuheshimu makubaliano hayo
Serikali ya DRC na M23 pia walikubaliana kutekeleza makubaliano hayo kama msingi wa majadiliano zaidi ya kurejesha amani mashariki mwa Congo na katika eneo la Maziwa Makuu.
Mazungumzo yajayo yataangazia mizizi ya mzozo huo na jinsi ya kuupatia suluhisho la kudumu.
Mazungumzo ya Doha pia yalipelekea serikali kukubali kuzingatia makubaliano yote wakati majadiliano yanaendelea.
Makubaliano haya ya kusitisha mapigano yanakuja huku mapigano makali yakiripotiwa kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23 katika maeneo ya Walikale. Ripoti pia zinaonyesha kuwa M23 imeanza kuimarisha ngome zake karibu na Walikale-Centre, hatua inayoashiria kuwa huenda ikawa na nia ya kurejea mjini humo, walikoondoka mwezi uliopita.


