Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda umezidi kuzorota baada ya serikali ya Kigali kutangaza kujiondoa kutoka kwenye Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (CEEAC), kama ilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari siku ya Jumapili tarehe 8 Juni.
Uamuzi huu wa Rwanda umekuwa chanzo kingine cha mvutano na Congo, huku suluhisho la kudumu kuhusu hali ya ukosefu wa usalama Mashariki mwa DRC likiwa bado halijapatikana.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alisema kuwa sababu ya kujitoa kwa Rwanda ni kwamba jumuiya hiyo imegeuzwa kuwa chombo cha kufanikisha malengo ya DRC.
Majadiliano ya kurejesha amani Mashariki mwa Congo yanaendelea kwa kusuasua, japokuwa mchakato uitwao “Mfumo wa Washington” umeshawasilisha rasimu ya makubaliano kwa Rwanda na DRC, rasimu iliyotokana na mapendekezo ya pande zote mbili.
Wataalamu kutoka nchi hizo mbili wanatarajiwa kukutana wiki hii jijini Washington kuijadili rasimu hiyo kabla ya kuidhinishwa rasmi na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili.
Lengo kuu ni kufungua njia ya makubaliano ya amani kati ya Rais Félix Tshisekedi wa Congo na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Hata hivyo, mazungumzo kati ya serikali ya Congo na waasi wa AFC/M23 yaliyofanyika Doha, Qatar, yalivunjika baada ya siku 32 bila mafanikio, jambo lililowafanya wajumbe wa M23 kujiondoa na kurejea Goma Ijumaa iliyopita.
Ingawa bado hakuna hatua kubwa iliyopigwa, kuna matumaini kuwa mazungumzo yataanza upya pande zote mbili zikikubaliana juu ya masharti muhimu kabla ya kuingia mezani.
Katika mahojiano maalum na shirika la habari la serikali, Waziri Nduhungirehe alisema kwamba licha ya kuwepo njia mbalimbali za kutafuta amani, Congo inazivuruga makusudi.
Alisema: “Congo inazidi kulalamika dhidi ya Rwanda kwenye mashirika ya kimataifa na kikanda, jambo ambalo linaathiri mazungumzo ya amani. Kumbukeni kuwa Rais Kagame alikutana na Rais Tshisekedi Doha, Qatar tarehe 18 Machi.”
Waziri huyo alieleza kuwa mwenendo wa serikali ya DRC unatia mashaka kama kweli wanataka amani, licha ya kusaini makubaliano ya msingi Washington na sasa wakiwa kwenye mazungumzo kuhusu mkataba kamili wa amani.


