Marekani, kupitia idara yake ya Uhamiaji na Forodha (ICE), imemkamata Ribvar Karimi, aliyewahi kuwa sniper katika jeshi la Iran kati ya mwaka 2018 hadi 2021.
Karimi alikamatwa Jumapili katika mji wa Locust Fork, jimbo la Alabama, ambako alikuwa akiishi na mke wake Mmarekani.
Wakati wa kukamatwa kwake, Karimi alipatikana na kitambulisho cha kijeshi cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama ilivyothibitishwa na Wizara ya Usalama wa Ndani (DHS).
Ingawa aliingia Marekani kwa visa ya mchumba mnamo Oktoba 2024, hakufuata mchakato wa kubadili hadhi yake ya uhamiaji, hali iliyomfanya aishi nchini kinyume cha sheria.
Katika uchunguzi mwingine, ICE pia ilimkamata Mehran Makari Saheli, mwenye umri wa miaka 56, aliyewahi kuwa mwanachama wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran, na ambaye alikiri kuwa na uhusiano na Hezbollah. Ingawa alihukumiwa kifungo cha miaka 15 kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria, aliendelea kujificha baada ya kuamriwa kuondoka nchini mwaka 2022.
Watu wengine wawili waliotuhumiwa kwa vitendo vya ukatili pia walikamatwa: mmoja huko Arizona akiwa na bastola ya 9mm, na mwingine kwa tuhuma za ukatili wa familia.
Wote wamewekwa kizuizini na ICE wakisubiri kurejeshwa makwao. Mke wa Karimi, ambaye ni mjamzito wa miezi saba, alisema kuwa mumewe anapenda Marekani na hakuwa na nia yoyote mbaya.


