Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, amechaguliwa tena kama Mwenyekiti wa chama tawala cha NRM (National Resistance Movement), huku akijiandaa kuwania urais tena mwaka 2026.
Katika hotuba yake huko Kampala baada ya kuthibitishwa kuwa mgombea rasmi, Museveni alitaja vipaumbele sita atakavyovifanyia kazi katika muhula wake mpya wa miaka sita: amani, maendeleo, utajiri, ajira, huduma, na masoko.
Alisema:
“Niko hapa kuelezea zaidi umuhimu wa mambo haya sita kwa Waganda. Amani si tu kutokuwa na vita, bali pia ni kupambana na uhalifu. Maendeleo ni barabara, umeme, shule na zaidi. Utajiri uifikie kila kaya, ajira ziongezeke, huduma ziboreke na masoko yafunguliwe zaidi.”
Museveni aliongeza kuwa sababu nyingine ya kuwania tena ni kukuza viongozi watakaosaidia kuondoa Uganda kutoka kwa hali ya nchi inayoendelea (GDP ya dola bilioni 66) hadi kuwa nchi yenye uchumi mkubwa wenye GDP ya dola bilioni 500 katika miaka ijayo.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani kwa rasilimali za Uganda kama njia ya kuongeza mapato na kuunda ajira.
“Tunachopaswa kufanya ni kuchakata tunavyovyozalisha: dhahabu, shaba, kahawa, kunde na vinginevyo badala ya kuviuza ghafi. Hii ndiyo njia ya kuvutia viwanda na kukuza uchumi wetu,” aliongeza.


