Bwana Lungele Mbiso, aliyekuwa mkuu wa mawasiliano katika ofisi ya Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini upande wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayoongozwa na Jean Jaques Perusi katika Wilaya ya Uvira, anaripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi kifuani na mwanajeshi wa FARDC na kufa papo hapo.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki hii iliyopita, ambapo mwanajeshi wa FARDC mwenye cheo cha Kapteni alipiga risasi na kumuua huyu mfanyakazi wa ofisi ya Gavana wa Kivu Kusini. Wananchi waliokuwa na hasira walimshambulia kwa mawe na fimbo hadi kumuua.
Inasemekana kuwa tukio hilo lilitokana na mabishano yaliyotokea kati ya wafanyakazi wa Gavana na wanajeshi, ingawa chanzo halisi cha mabishano hakikufafanuliwa.
Tukio hilo lilitokea Uvira, mji ambao kwa sasa ndio makao makuu ya muda ya Jimbo la Kivu Kusini baada ya waasi wa AFC/M23 kuchukua mji wa Bukavu tarehe 16 Februari 2025, mji unaochukuliwa kama makao makuu ya jimbo hilo.
Kwa sasa, Bukavu iko chini ya udhibiti wa AFC/M23, ambao tayari wameanzisha miundo ya kiutawala kuanzia ngazi ya mkoa hadi kwa viongozi wa mitaa.
Hili limetokea wakati serikali ya Kongo inaendelea kupeleka wanajeshi wengi zaidi katika eneo hilo, wakiwemo mamluki waliotoka Colombia kwa ajili ya kusaidia katika mapambano dhidi ya kundi la waasi wa M23.
Hali hii inazidisha mvutano wa vita, ambapo serikali inaripotiwa kuwa inajiandaa kushambulia kwa nguvu maalum ili kurejesha miji mikubwa kama Goma na Bukavu, ambayo iko karibu na Uvira.
Hii inajiri wakati serikali ya Kongo imesaini makubaliano ya amani na Rwanda, makubaliano yaliyolenga kumaliza kabisa migogoro ya vita ya muda mrefu mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na Uvira ambako mipango hiyo ya kijeshi inaendelea.


