Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliwasili DR Congo siku ya Alhamisi kwa ziara ya siku tatu, shirika hilo la dunia lilisema, huku mapigano makali na waasi wa M23 yakiendelea katika eneo la mashariki .
Kundi la M23 limeteka maeneo mengi katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu kuanza kumiliki silaha tena mwishoni mwa 2021.
Wapiganaji wa M23 pia wamesonga mbele katika siku za hivi karibuni, na kutishia kukata njia zote za kuelekea Goma, jiji lenye zaidi ya watu milioni moja kwenye mpaka wa Rwanda.
Ujumbe huo ulipaswa kukutana na Rais Felix Tshisekedi kabla ya kusafiri kwenda Goma siku ya Jumamosi.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC unaojulikana kwa jina la MONUSCO umesema lengo la ziara ya baraza hilo ni kutathmini hali ya usalama na kibinadamu katika eneo la Kivu Kaskazini.
“Tuko hapa kuunga mkono hatua ya MONUSCO, kukumbusha kuwa ni sehemu ya suluhu la kutafuta amani,” alisema balozi wa Umoja wa Mataifa wa Gabon Michel Xavier Biang alipowasili Kinshasa.
Kikosi cha kulinda amani ni mojawapo ya misheni kubwa na ya gharama kubwa zaidi ya Umoja wa Mataifa duniani, ikiwa na zaidi ya wafanyakazi 16,000 waliovaa sare.
Wakaazi wanaishutumu kwa kushindwa kukabiliana na makumi ya makundi yenye silaha yanayoendesha harakati zake mashariki mwa DRC, wakiwemo waasi wa M23.
Juhudi kadhaa za kikanda zilizokusudiwa kusuluhisha mzozo zimeshindwa.
Usitishaji mapigano uliosimamiwa na Angola uliokuwa unafaa kuanza kutekelezwa Jumanne ulisambaratika siku hiyo hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikuwa amewataka waasi kuzingatia usitishaji huo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia alitishia vikwazo dhidi ya vyama ambavyo havikuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.
Serikali ya DRC inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, Marekani na mataifa mengine kadhaa ya magharibi, pia wamehitimisha kuwa Rwanda inaunga mkono kundi hilo, ingawa Kigali imekanusha hilo.
Mapigano kati ya jeshi la DRC na M23 yamewakosesha makazi takriban watu 800,000.


