Mtoto wa kiongozi wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema ananuia kugombea urais mwaka 2026, ikiwa ni mara ya kwanza kwa jenerali huyo kutoa ratiba ya kuchukua nafasi ya babake ambaye ameiongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa miaka 37 .
Upinzani nchini Uganda kwa muda mrefu umekuwa ukimshutumu Museveni kwa kutaka kuweka utawala wa kifalme nchini Uganda na kudai kuwa alikuwa akimtayarisha mwanawe Muhoozi Kainerugaba kuchukua nafasi yake. Museveni amekanusha tuhuma hizo.
Hivi sasa ni mshauri maalum wa rais kwa operesheni maalum, jenerali huyo mwenye umri wa miaka 48 anajulikana kwa kurusha ujumbe wa kutatanisha ambao umemfanya akaripiwe na babake.
Kainerugaba alifuta haraka jumbe hizo kuhusu matarajio yake ya urais, ambazo alikuwa amezichapisha kwenye Twitter siku ya Jumatano.
“Mumetaka niseme milele! Sawa, kwa jina la Yesu Kristo Mungu wangu, kwa jina la vijana wote wa Uganda na ulimwengu na kwa jina la mapinduzi yetu makubwa, nitasimama kugombea Urais katika 2026,” Kainerugaba aliandika.
Katika tweet nyingine, alionyesha kutokuwa na subira kwa kusubiri kwa muda mrefu kuchukua nafasi ya baba yake.
“Waziri Mkuu wa Uingereza ana umri wa miaka 42, Waziri Mkuu wa Finland ana miaka 37. Baadhi yetu tunapiga miaka 50. Tumechoka kusubiri milele,” alisema.
Awali Kainerugaba aliwahi kuwa kamanda wa majeshi ya nchi kavu lakini aliondolewa katika nafasi hiyo baada ya kutishia kuivamia nchi jirani ya Kenya, jambo ambalo baadaye alisema ni mzaha.
Museveni bado hajasema iwapo ana nia ya kugombea tena 2026, ingawa wafuasi wake wamemtia moyo kufanya hivyo.


