Mnamo Alhamisi, Julai 10, mapigano makali yalizuka katika eneo la Mitembe/Katobo, katika Banamulindwa (groupement ya Kisimba), wilayani Walikale, mkoani Kivu Kaskazini, kati ya waasi wa AFC/M23 na wapiganaji wa kujitolea wanaojiita Wazalendo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ACTUALITE.CD, waasi wa AFC/M23 waliokuwa Ihula walishambulia kambi za Wazalendo huko Matembe mnamo saa mbili asubuhi kwa saa za huko. Hata hivyo, walirudishwa nyuma hadi Ihula. Inaripotiwa kuwa mapigano hayo yalidumu kwa saa kadhaa, ingawa idadi ya waliokufa haijulikani bado.
Asubuhi ya Ijumaa, hali ilikuwa shwari katika eneo hilo, na inasemekana kwa sasa eneo lipo chini ya udhibiti wa Wazalendo.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza kuwa mivutano bado ipo, na hali ya usalama inaweza kuzorota wakati wowote kutokana na kuongezeka kwa shughuli za waasi katika eneo la Walikale.
Wakazi wa Mitembe tayari walikuwa wamekimbilia Pinga tangu vurugu zilipoanza kwenye eneo hilo.


