Wajumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda walitarajiwa wiki hii mjini Washington kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mgogoro wa mashariki mwa Kongo. Taarifa zinasema tayari wamewasili na wameshaanza kazi, wakikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu Marekani iingilie kati mgogoro huo.
Lengo lao ni kufikia makubaliano yatakayowasilishwa kwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote mbili.
Hakuna tarehe rasmi iliyotangazwa ya kutiwa saini kwa mkataba huo, lakini Marekani inatarajia mkataba huo utasainiwa kabla ya mwezi Julai, kulingana na ripoti ya Radio France Internationale (RFI).
Habari zinaeleza kuwa mazungumzo hayafanyiki tena kupitia wapatanishi wa Kimarekani au ujumbe wa WhatsApp; kwa siku mbili hadi tatu zilizopita, wataalamu wa Kongo na Rwanda wamekuwa wakikutana ana kwa ana mjini Washington.
Mkataba ulioko mezani kwa sasa ni toleo la pili, lililoandaliwa na waratibu kutoka Marekani kulingana na maoni ya awali kutoka pande zote mbili.
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alitoa maoni yake jana kupitia mtandao wa X kuhusu mazungumzo hayo.
Alisema: “Mwanzoni, Marekani walitarajia makubaliano yafikiwe katikati ya Juni, lakini lengo hilo la awali […] lilipaswa kuendana na hali halisi ya mazungumzo.”
Inatarajiwa kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Kongo watakutana tena Washington baada ya wataalamu kukubaliana juu ya mkataba wa msingi, kabla ya mkutano wa viongozi wakuu wa nchi hizo mbele ya Donald Trump.
Hakuna ratiba kamili imetangazwa hadi sasa, lakini Marekani inasukuma kwa kasi kubwa, ikitumaini mchakato utakamilika kufikia Julai, kama ripoti za RFI zinavyobainisha.
Waziri Nduhungirehe alisisitiza tena kwenye mitandao ya kijamii kuwa makubaliano yoyote yatakayofikiwa lazima yalete amani yenye manufaa kwa pande zote mbili, huku mazungumzo yakiendelea.


