GCjJqDpXUAAgq5f_1

Rais Ndayishimiye Aendelea Kudai Kuwa Rwanda Inapanga Kuvamia Burundi

Sangiza iyi nkuru

Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, amesisitiza tena kuwa anazo taarifa za uhakika kuwa Rwanda bado inapanga kushambulia nchi yake.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahojiano na mwandishi wa habari Marc Perelman wa televisheni ya France 24.

Mwezi uliopita, Ndayishimiye alipokuwa akizungumza na BBC, alisema tayari anayo taarifa kwamba Rwanda ina mpango wa kuzusha vita dhidi ya Burundi, na akatoa onyo kuwa “Rwanda likithubutu kushambulia Bujumbura kupitia Congo, nasi hatutafika Kigali kupitia Kirundo.”

Alipoulizwa na France 24 kama bado anaamini Rwanda ina mpango huo wa kushambulia Burundi, Ndayishimiye alithibitisha kwamba hali hiyo bado ipo, na kuna ushahidi unaoonyesha hivyo.

Alisema: “Kwanza kabisa, tuna taarifa za kiintelijensia, tunaufahamu huo mpango, na pia kuna viashiria vya wazi. Moja ya ushahidi ni kwamba Rwanda inawapa hifadhi wahusika wa jaribio la mapinduzi la mwaka 2015 ambao sasa wanapanga kuvamia Burundi.”

Aliendelea kusema kuwa Rwanda inaweza kuwatumia watu hao kama wanavyotumia waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuwaita Wacongo, ilhali wao ni watu wanaotumiwa na Rwanda.

“Wana mpango wa kuwatumia waliohusika kwenye jaribio la mapinduzi mwaka 2015, kwa kuwaita Waburundi, ilhali ni Rwanda ndiyo itakuwa nyuma ya mashambulizi hayo,” alisema.

Rais Ndayishimiye pia alisema serikali yake inahofia Rwanda kukataa kuwakabidhi watu hao waliohusika na jaribio la kumpindua hayati Rais Pierre Nkurunziza ili wafikishwe mbele ya sheria, lakini akabainisha kuwa kwa sasa Rwanda haina nafasi ya kufanya shambulio hilo mpaka mapigano mashariki mwa DRC yatakapomalizika.

Akaongeza kuwa Burundi itaendelea kuwa macho hadi itakapopata uthibitisho wa wazi kuwa Rwanda haina tena nia ya uadui dhidi ya Burundi.

Mpaka sasa, serikali ya Rwanda haijajibu rasmi tuhuma hizo mpya zilizotolewa na Rais wa Burundi.

Mwezi Machi mwaka huu, wakati Ndayishimiye aliposema wazi kuwa kuna mpango wa kuvamia Kigali, msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alisema walishangazwa na kauli hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa vyombo vya usalama vya nchi hizo mbili vilikuwa vinaendelea na mazungumzo kuhusu ulinzi wa mipaka yao ya pamoja.

Mahusiano kati ya Rwanda na Burundi yalianza kuzorota tena mwishoni mwa mwaka 2023 baada ya Burundi kuishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la Red Tabara linalopinga serikali ya Gitega.

Tension ilizidi baada ya Burundi kupeleka wanajeshi wake DRC kusaidia majeshi ya FARDC na FDLR katika vita dhidi ya M23. Baadaye, Rais Ndayishimiye akiwa mjini Kinshasa alitangaza kuwa ataunga mkono mpango wa kupindua serikali ya Rwanda kama njia ya kuwasaidia vijana wa Rwanda kujikomboa.

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *