Mchezaji wa kati kutoka Uganda, Ronald Ssekiganda, ameaga rasmi klabu ya Villa SC aliyokuwa akiiongoza kama nahodha. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 anajiunga na klabu ya APR FC ya Rwanda, baada ya kufikia makubaliano ya kuichezea kwa kipindi cha miaka miwili.
Kupitia ujumbe alioutuma kwa mashabiki na viongozi wa Villa SC, Ssekiganda alitoa shukrani kwa upendo alioonyeshwa na fursa ya kushinda taji la 17 la Ligi Kuu ya Uganda. Alisema anaondoka ili kuendelea kukua kama mchezaji.
Ssekiganda alichezea Villa SC tangu mwaka wa 2020, akifunga mabao matano katika mechi 69. Pia alihusika pakubwa kusaidia timu ya taifa ya Uganda kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika la mwaka 2025 litakalofanyika nchini Morocco.
Anatarajiwa kuimarisha safu ya kati ya uwanja wa APR FC, ambayo inaendelea kujijenga wakati wa dirisha la usajili wa wachezaji.


