Wataalamu wa kiufundi kutoka Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekamilisha rasimu ya makubaliano ya amani ambayo mataifa hayo mawili yanatarajiwa kuyasaini mwishoni mwa mwezi Juni.
Wataalamu hao waliandaa rasimu hiyo mjini Washington D.C., Marekani, ambako walifanya mazungumzo ya ana kwa ana kwa siku tatu.
Majadiliano yao yalilenga masilahi ya pamoja kati ya Kigali na Kinshasa, hasa katika nyanja za kisiasa, usalama, na uchumi.
Jumatano tarehe 18 Juni, walikamilisha nyaraka ya rasimu hiyo katika hafla iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Allison Hooker.
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Hooker alisema anajivunia kuongoza majadiliano yaliyowezesha maandalizi ya mkataba huo wa amani, akiyataja kuwa hatua muhimu kuelekea amani ya kudumu.
Alisema:
“Ninajivunia kuongoza mazungumzo ya amani ya siku tatu yaliyozaa matunda ya kusainiwa kwa rasimu ya makubaliano ya amani kati ya wawakilishi wa DRC na Rwanda. Wiki ijayo tunatarajia kupokea Mawaziri wa Mambo ya Nje tarehe 27 Juni kwa ajili ya kutia saini, chini ya uongozi wa Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio. Kwa pamoja, tunafanya kazi kuelekea amani ya kudumu na usalama wa kweli katika eneo hili.”
Tarehe 27 Juni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Balozi Olivier Nduhungirehe na mwenzake wa DRC Thérèse Kayikwamba Wagner watatia saini mkataba huo wa amani mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio.
Rasimu ya makubaliano hayo imejengwa juu ya makubaliano ya awali yaliyosainiwa na mataifa hayo mawili tarehe 25 Aprili 2025.
Mambo yaliyokubaliwa ni pamoja na kuheshimu mipaka ya kila nchi na kusitisha mapigano; kuvunja, kupokonya silaha, na kuwaunganisha tena wapiganaji wa makundi yasiyo ya kiserikali; kuanzisha chombo cha pamoja cha usalama; kurahisisha urejeo wa wakimbizi na waliopoteza makazi.
Pia kunajumuishwa kurahisisha misaada ya kibinadamu na kuweka mpango wa kuunganisha uchumi wa kikanda.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuwa Qatar, kama moja ya nchi zinazosaidia Rwanda na DRC katika mazungumzo haya, nayo ilishiriki katika mazungumzo ya hivi karibuni ili kuhakikisha kuwa yanalingana na mipango ya Kigali na Kinshasa ya kuleta amani.
Mbali na kutiwa saini kwa mkataba huo wa amani mwishoni mwa mwezi huu, Marekani pia inatarajia marais wa Rwanda na DRC watakutana mjini Washington “kama sehemu ya kuendeleza amani, utulivu, na maendeleo ya kiuchumi katika Ukanda wa Maziwa Makuu.”


