Rais Donald Trump wa Marekani ameidhinisha mpango wa kuivamia Iran, lakini bado hajafanya uamuzi wa mwisho wa kuitekeleza, kulingana na taarifa ya CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani.
Taarifa kutoka kwa mashirika ya kijasusi zilizotolewa kwa CBS zinasema kuwa Rais wa Marekani alisita kutoa amri ya kushambulia huku Iran bado ikiwa na nafasi ya kusitisha mpango wake wa nyuklia. Inasemekana Trump anafikiria shambulio la kijeshi kwenye kiwanda cha usindikaji wa uranium nchini Iran.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, siku ya Jumatano alikataa ombi la Trump la kuachana na mpango huo, baada ya rais huyo wa Marekani kusema kwamba uvumilivu wake umeisha.
Jumatano hiyo hiyo, Trump alipoulizwa kama Marekani inaweza kuingia vitani na Iran, alijibu: “Naweza kufanya hivyo, pia si lazima nifanye.”
Siku hiyo hiyo, Khamenei alimshambulia Trump kwa maneno katika hotuba yake, akisema kuwa “uingiliaji wa kijeshi wa Marekani” utagharimu sana, na akaongeza: “Iran haitasalimu amri.”
Trump naye alimtakia “bahati njema,” lakini alikataa kufichua mipango yake ya baadaye, akisema: “Nataka kuwa wa kushangaza; hakuna anayejua nitakachofanya.”
Vita kati ya Iran na Israel—ambavyo Marekani inataka kujiunga navyo—vinatazamiwa kuingia wiki ya pili kufikia Ijumaa ijayo, huku nchi hizo mbili za Mashariki ya Kati zikiendelea kurushiana makombora, na raia wa kawaida wakiendelea kuumia katikati ya mapigano.


