Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Uganda imetoa onyo kwa raia wake kutofanya vipimo vya DNA, ikisema kuwa matokeo yake huumiza kihisia kwa kiasi kikubwa.
Msemaji wa wizara hiyo, Simon Mundeyi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna ongezeko kubwa la watu wanaotaka kujua uhusiano wa damu kati yao na watoto wanaowalea.
Alisema kwamba katika siku tatu zilizopita, kituo kimoja cha vipimo vya DNA kilipokea watu 94—95% wakiwa wanaume waliotaka kuthibitisha kama watoto wanaowalea ni wao, 3% wanawake, na 2% watoto waliotaka kujua wazazi wao halisi.
Kutokana na ongezeko hilo, wizara hiyo imeshauri wananchi wenye mioyo laini kuepuka vipimo hivyo, kwa kuwa 98% ya matokeo yanakuwa hasi, yaani hakuna uhusiano wa damu unaothibitishwa.
Alisema:
“Tunaona watoto wakubwa wakitaka kuthibitisha kama wale wanaowaita wazazi kweli ndio waliowazaa. Lakini nawaonya Waganda: msifanye kipimo cha DNA kama huna moyo mgumu.”
Akaongeza:
“Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa 98% ya matokeo ni hasi. Fikiria mwanamume aliyemlea mtoto kwa miaka 15 kisha apate kujua si wake. Hilo husababisha mshtuko mkubwa, hasa kwa mtoto. Ili kuepuka hali hiyo, tafadhali msifanye. Endeleeni kuishi na mwisho wake mufe kwa amani.”


