Jeshi la Iran limeanzisha mashambulizi dhidi ya Israel kwa kutumia drones, kama njia ya kulipiza kisasi kufuatia shambulio la hivi karibuni lililotekelezwa na Israel dhidi yao.
Mashambulio hayo ya Israel yanadaiwa kumuua Kamanda wa Vikosi vya Ardhi vya Iran, kiongozi wa kikosi maalum cha jeshi kinachojulikana kama IRGC, pamoja na kamanda wa vikosi vya dharura.
Ripoti zinaonyesha kuwa, kama kisasi, Iran imetuma drones zaidi ya 100 na makombora kuelekea Israel.
Vyombo vya habari vya kimataifa vikiwemo Televisheni ya Al Jazeera vimeripoti kuwa majeshi ya Israel na Jordan yameanza kuangusha drones hizo.
Televisheni ya taifa ya Israel inasema kwamba jeshi lake linaziangusha drones hizo katika anga ya Syria, huku Channel 12 ikiripoti kuwa baadhi yao zinaangushwa katika anga ya Saudi Arabia.
Shirika la habari la taifa la Jordan nalo limethibitisha kuwa nchi hiyo iliweza kuangusha drones na makombora yaliyoingia kwenye anga yake siku ya Ijumaa.


