Marekani imelitaja tena Rwanda, ikilitaka kuondoa wanajeshi wake wanaodaiwa kuwepo kwenye ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kauli hiyo imetolewa na Massad Boulos, mshauri maalum wa aliyekuwa Rais Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika.
Akiwahutubia wanahabari siku ya Alhamisi, Boulos alisema:
“Tunasimamia msimamo wetu thabiti: Rwanda inapaswa kusitisha msaada wowote wa kijeshi kwa M23 na kuondoa wanajeshi wake wote walioko kwenye ardhi ya Congo.”
Awali mwezi huu, Boulos alitembelea Kigali ambapo alipokelewa na kufanya mazungumzo na Rais Paul Kagame. Alieleza matumaini kwamba pande zote zinazohusika kwenye mgogoro wa mashariki mwa Congo zitaweza kufikia suluhu ya haraka na ya amani.
Marekani ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikiishinikiza Rwanda, kwa kuituhumu kuisaidia kijeshi kundi la waasi la M23 ambalo limekuwa kwenye mapigano na serikali ya Kinshasa kwa zaidi ya miaka mitatu.
Mnamo Februari mwaka huu, Washington iliweka vikwazo dhidi ya Jenerali mstaafu James Kabarebe, ambaye ni mshauri mkuu wa masuala ya ulinzi na usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda, kwa madai ya kuongoza misaada ya Rwanda kwa kundi la M23.
Kwa upande wake, Kigali imekuwa ikikanusha kuwa na wanajeshi mashariki mwa DRC, ingawa inathibitisha kuwa ina vikosi vya ulinzi mpakani kama tahadhari dhidi ya tishio lolote kutoka Congo.


