Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetangaza kuwa itaanza mchakato wa kisheria dhidi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila Kabange, kwa tuhuma za usaliti wa kiwango cha juu.
Kinshasa imetoa tangazo hili saa chache tu baada ya Kabila kurejea kutoka Zimbabwe alikokuwa ameishi uhamishoni, na kufika katika jiji la Goma ambalo kwa sasa lipo mikononi mwa waasi wa M23.
Katika taarifa iliyotolewa usiku uliopita, Waziri wa Sheria wa DRC alieleza kuwa Mkuu wa Ukaguzi wa Jeshi (FARDC) pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Rufaa tayari wameanzisha mchakato wa kumfungulia mashitaka Kabila.
Waziri Constant Mutamba alimtuhumu Kabila kwa “ushiriki wa moja kwa moja katika uvamizi unaofanywa na Rwanda kupitia kundi la kigaidi la AFC/M23”.
Kabila bado hajazungumza hadharani kuhusu kurejea kwake nchini wala kuhusu tuhuma zinazomkabili kutoka kwa serikali ya Kinshasa. Hata hivyo, mara kadhaa amekanusha madai kuwa ndiye mfadhili mkuu wa M23, kama inavyodai serikali.
Wakati huo huo, msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, alisema kuwa hakuna tatizo kwa Joseph Kabila kuwepo katika jiji la Goma linalodhibitiwa na kundi hilo.
Mbali na kumfungulia mashitaka, Waziri Mutamba pia alisema kuwa serikali imetoa maagizo ya kukamata mali zote za Kabila – zikiwemo zile zinazohamishika na zisizohamishika – pamoja na kuweka vizuizi vya kusafiri kwa watu wote wanaoshirikiana naye katika kitendo hiki cha “usaliti wa hali ya juu”.
Serikali ya DRC imeeleza kuwa tayari imekamata mali za Kabila katika maeneo ya Kingakati, Kashamata, GLM na sehemu nyingine.
Aidha, kupitia taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shabani Lukoo Bihango, ilitangazwa kuwa shughuli zote za chama cha PPRD cha Kabila zimesitishwa kote nchini kutokana na madai ya ushiriki wa kiongozi huyo katika vita vinavyoendelea.
Hadi sasa, chama hicho hakijatoa tamko lolote rasmi kuhusu hatua hiyo.
Kabila, mwenye umri wa miaka 53, ambaye kwa sasa ni seneta wa DRC, aliiongoza nchi hiyo kwa miaka 18 kuanzia mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent-Désiré Kabila.
Kundi la waasi la M23, ambalo Kabila anatuhumiwa kushirikiana nalo kati ya mwaka 2012 na 2013, liliwahi kupigana na jeshi la DRC ambalo yeye alikuwa kamanda wake mkuu. Hata hivyo, kundi hilo lilishindwa na wanachama wake walikimbilia Uganda na Rwanda.


