Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kilitangaza Jumamosi kuwa kiongozi wao mashuhuri Tundu Lissu, aliyekamatwa kwa tuhuma za udanganyifu, alihamishiwa gereza jingine – siku moja baada ya chama hicho kusema kuwa hawajui alipo.
Kukamatwa kwa Lissu kumezua upya mjadala kuhusu rekodi ya Rais Samia Suluhu Hassan katika masuala ya haki za binadamu, hasa anapojiandaa kugombea muhula wa pili ifikapo mwisho wa Oktoba.
Rais Samia amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake imejikita katika kulinda haki za binadamu na kuendeleza utawala bora.
Msemaji wa CHADEMA, Brenda Rupia, alisema kuwa viongozi wa chama walikutana na maafisa wa magereza na kuelezwa kuwa Lissu amehamishwa.
“CHADEMA inawataarifu wananchi kuwa Tundu Lissu amepelekwa Gereza la Ukonga,” alisema Rupia.
Msemaji wa Huduma za Magereza Tanzania, Elizabeth Mbezi, hakupatikana kwa simu wala kujibu ujumbe mfupi kuhusu suala hilo, kwa mujibu wa BBC.
Ijumaa, CHADEMA ilitangaza kuwa viongozi wa chama, mawakili wa Lissu na familia yake walijaribu kumwona katika gereza la Dar es Salaam ambako alikuwapo tangu Aprili 10, lakini hawakuweza kumpata.


