Serikali ya Uholanzi imetangaza kuwa inafunga baadhi ya balozi zake na ofisi za ubalozi mdogo (konseli) katika mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Burundi, ili kupunguza matumizi ya bajeti.
Taarifa hii ilithibitishwa kupitia barua ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Caspar Veldkamp, aliyoiwasilisha kwa Bunge la nchi hiyo.
Katika barua hiyo, aliandika: “Ninapanga kufunga balozi tano na konseli mbili: Bujumbura (Burundi), Havana (Cuba), Juba (Sudan Kusini), Tripoli (Libya), Yangon (Myanmar), pamoja na konseli za Antwerp na Rio de Janeiro.”
Hatua hiyo inalenga kuokoa kiasi cha dola milioni 25 huku serikali ya Uholanzi ikipanga kupunguza matumizi ya wizara zake kwa asilimia 25.
Uamuzi wa kufunga ubalozi wa Bujumbura umeibua maswali kwani Uholanzi imekuwa kati ya wafadhili wakuu wa Burundi kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, mwaka 2022 Uholanzi ilitoa msaada wa takribani dola milioni 39.9 kwa Burundi.
Kati ya 2023 hadi 2027, Uholanzi pia ilikuwa imeahidi msaada wa Euro milioni 160 kusaidia sekta za usalama wa chakula, afya ya uzazi, haki za binadamu na ajira kwa vijana nchini Burundi.


