Wanajeshi 12 wa jeshi la Burundi wamezama na kupoteza maisha katika Ziwa Tanganyika wiki iliyopita baada ya boti yao ya kijeshi kupata ajali.
Ajali hiyo ilitokea siku ya Ijumaa tarehe 18 Aprili 2025, wakati boti ndogo ya haraka ya jeshi la majini la Burundi ilipopata dhoruba kali na kuzama. Boti hiyo ilikuwa na wanajeshi kadhaa, wengi wao wakiwa walijeruhiwa katika mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako Burundi ina vikosi vyake.
Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Burundi, wanajeshi tisa kati ya waliokuwamo ndani ya boti hiyo walikuwa majeruhi wa vita kutoka mashariki mwa Kongo.
Ajali hiyo ilitokea karibu na Kisiwa cha Ubwali, kilicho katika Ziwa Tanganyika, ambapo kuna kambi ya kikosi cha jeshi la Burundi.
Mamlaka za kijeshi zimesema ajali ilisababishwa na mawimbi makali yaliyokumba ziwa hilo wakati huo.
Hadi Jumamosi jioni, hakuna miili yoyote iliyokuwa imepatikana, licha ya juhudi za uokoaji kuendelea kufanywa na kikosi cha majini cha Burundi.


