Kamanda Mkuu wa Jeshi la Uganda (UPDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amemjibu mfuasi wake kwenye X (zamani Twitter) aliyemshauri acheze karata ya kumuoa Miss Jolly Mutesi kama mke wa pili. Akijibu kwa utani, alisema kuwa jambo hilo lingemgharimu maisha kwa mkono wa mke wake Charlotte.
Kisa kilianza baada ya Muhoozi kuposti picha akiwa pamoja na Rais Paul Kagame huku akiandika: “Tutashinda maadui wote. Mungu awabariki mashujaa.” Mashabiki wake kwenye mtandao huo walifurika sehemu ya maoni, mmoja akimtania: “Muhoozi njoo umchukue bibi yako (Jolly Mutesi) awe mke wa pili.”
Gen Muhoozi alijibu haraka: “Unataka Charlotte aniue.”
Kauli hiyo ilizua mijadala mingi mitandaoni — baadhi wakijiuliza mbona mtu mwenye nguvu kama yeye awe na hofu ya kifo, wengine wakicheka na kusema ni ishara ya mapenzi ya dhati kwa mke wake.
Taarifa za uhusiano wa karibu kati ya Muhoozi na Jolly Mutesi ziliibuka mwaka 2022, wakati Jenerali alipomwalika Miss Mutesi kwenye sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake. Hata hivyo, Miss Mutesi alimjibu kuwa hatoweza kuhudhuria, lakini angemkumbuka siku nyingine.
Kwa kumbukumbu, Jenerali Muhoozi, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, ameishi kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka 25 na Charlotte, na wamejaliwa watoto wanne.


