Jumamosi hii tarehe 3 Mei, Jeshi la Polisi la Rwanda limewaaga rasmi kwa heshima maafisa 150 wa polisi waliostaafu hivi karibuni.
Kati ya hao, walikuwemo maafisa wadogo 45 na sajini 105.
Wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika makao makuu ya Polisi ya Rwanda huko Kacyiru, Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi la Rwanda (DIGP), DCG Jeanne Chantal Ujeneza, aliwashukuru maafisa waliostaafu kwa uadilifu, nidhamu na moyo wa kujitolea waliouonesha wakati wote wa utumishi wao kwa taifa.

Alitoa shukrani pia kwa familia zao kwa kuwaunga mkono katika safari yao ya kazi, licha ya changamoto na majukumu yaliyowafanya kutokuwepo karibu nao mara nyingi.
Alisema:
“Ingawa mmeingia rasmi katika mapumziko ya uzeeni, jukumu la kulinda usalama wa nchi yetu linaendelea, na tutaendelea kushirikiana kama ilivyokuwa.”
DIGP Ujeneza aliwataka waendelee kuwa wazalendo, kuonesha mienendo bora na moyo wa kujitolea kwa ajili ya taifa, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi la Rwanda litaendelea kuwaona kama sehemu ya nguvu zake muhimu katika kuhakikisha usalama na maendeleo ya nchi.
CIP (mstaafu) Bernard Gahonzire, aliyewakilisha wastaafu wenzake, alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, kwa kuwaruhusu kustaafu kwa heshima.
Pia aliishukuru uongozi wa Jeshi la Polisi la Rwanda kwa kuwaunga mkono wakati wote wa utumishi wao, na kuwasaidia kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Alisema:
“Safari yetu ya kikazi imekuwa ya muda mrefu na tumejifunza mambo mengi ambayo yatatuongoza hata baada ya utumishi wetu rasmi kumalizika.”
Aidha, alisisitiza kuwa katika maisha yao mapya baada ya kazi, hawatasahau kiapo chao, bali wataendelea kuenzi nafasi waliyopewa ya kulisaidia taifa, na wataendelea kuchangia maendeleo na usalama wa nchi popote watakapohitajika.




