Polisi nchini Kenya wanawahoji watu watatu kufuatia tukio ambapo mwanaume alirusha kiatu kwa Rais William Ruto huko Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori.
Tukio hilo lilitokea wakati Rais Ruto alipokuwa akihutubia wakazi wa Kehancha siku ya Jumapili, Mei 4, 2025.
Polisi wamesema uchunguzi unaendelea na watu wengine wanaoshukiwa bado wanatafutwa.
Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya, Kipchumba Murkomen, amesema watu hao watatu walikamatwa ili kufanyiwa uchunguzi wa kina kubaini kama tukio hilo lilikuwa la bahati mbaya au lilikuwa njama ya kuhatarisha usalama wa rais.
Ripoti za awali za uchunguzi zinaonyesha kwamba tukio hilo huenda lilikuwa na sababu za kisiasa na lilipangwa kabla ya ziara ya rais.
Vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya vimeripoti kuwa tukio hilo lilitatiza kwa muda hotuba ya rais aliyekuwa katika ziara ya Migori.

Video fupi ya sekunde tano inayosambaa mtandaoni inaonesha mtu aliyekuwa kwenye umati akirusha kiatu kuelekea kichwani mwa Rais Ruto wakati alipokuwa akihutubia hadhara.
Rais Ruto alijaribu kukwepa kiatu hicho kilipomfikia.
Walinzi wa rais walikimbilia jukwaani mara moja na mkutano kusimamishwa kwa muda wa dakika chache.
Vikosi vya usalama vilianza mara moja kusambaratisha umati wa watu waliokuwa karibu na tukio hilo, ingawa rais alikuwa akiwaomba waache.


