Ripoti ambazo bado hazijathibitishwa rasmi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zinaeleza kuwa Waziri wa Michezo na Burudani, Didier Budimbu, ametia saini mkataba na klabu ya Ufaransa AS Monaco wa thamani ya dola milioni 1.6 kwa kila msimu.
Kwa mujibu wa Mediacongo, mkataba huu unachukuliwa kuwa wa muhimu barani Afrika, ukilenga hasa kuinua mchezo wa soka nchini DRC.
Pia kunatajwa kuwepo na kiasi cha euro 200,000 kwa ajili ya kugharamia safari zinazohusiana na shughuli za AS Monaco nchini humo.
Taarifa kutoka wizara hiyo zinaeleza kuwa 80% ya fedha hizo zitaelekezwa kwenye mafunzo ya michezo, huku 20% zikitarajiwa kutumika katika kuitangaza DRC kimataifa.
Ushirikiano huu unahusisha kubadilishana maarifa, hasa katika mafunzo ya kiufundi na kusaidia vipaji vya vijana wa Congo. Inasemekana kuwa mazungumzo yalidumu kwa miezi saba.
Baada ya kuwepo kwa manung’uniko, wizara imesisitiza kuwa mchakato huo ulikuwa wazi na kwamba Waziri Didier Budimbu hana maslahi binafsi kwenye makubaliano hayo.


