Nahodha wa timu ya Tottenham Hotspur, Son Heung-min, ameripoti kwa polisi wa Korea Kusini akimtuhumu mwanamke aliyemdanganya kuwa mjamzito kwa lengo la kumtapeli pesa nyingi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Korea Kusini kama Yonhap News Agency na The Korea Times, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 20 na mwanaume mwenye miaka 40 wako chini ya uchunguzi kwa kosa la kujaribu kutapeli.
Son anadai kuwa wawili hao walimwambia uongo kwamba mwanamke huyo ni mjamzito ili kumlazimisha awalipe fedha nyingi wasianike suala hilo hadharani. Amesema kitendo hicho ni udanganyifu mkubwa na ni aina ya unyang’anyi.
Timu ya wanasheria wa Son ilieleza kuwa mwanamke huyo alidai kuwa mjamzito kwa mara ya kwanza mwezi Juni 2024, na akaanza kumdai pesa nyingi ili anyamaze kimya.
Son Heung-min mwenye miaka 32 hajaoa wala hana mtoto. Amewahi kusema kuwa hataki kuwa na familia wala watoto hadi atakapostaafu soka, kwa sababu anataka kujitolea kikamilifu kwenye taaluma yake ya michezo.


