1748066608229

Mshangao wa Kisasa: Mabinti Wanaendelea Kupimwa Usichana Katika Nchi Hizi

Sangiza iyi nkuru

Katika mataifa mengi ya Afrika na Asia, bado kuna desturi ya kupima usichana kwa wasichana, hasa kabla ya ndoa au pale inapodaiwa kuwa msichana alibakwa — yote haya yakifanywa kwa nia ya kupata “ushahidi” kuwa msichana ni bikira.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kipimo cha ubikira kinahusisha kukagua utando mdogo ndani ya uke wa msichana unaoitwa hymen, ili kuangalia kama haujavunjika. Madaktari au hata watu wasiokuwa na mafunzo rasmi hutumia vidole vyao kukagua uke wa msichana.

Wanaounga mkono utaratibu huu hudai kuwa ni njia ya kuthibitisha uaminifu wa msichana kabla ya ndoa. Hata hivyo, WHO inasisitiza kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kwamba hymen iliyosalia nzima ni dalili ya kutokufanya ngono. Hymen inaweza kuchanika kwa sababu nyingi zisizohusiana na tendo la ndoa, kama vile michezo au ajali.

Wataalamu wa haki za binadamu wanakemea vikali desturi hii, wakisema kuwa ni udhalilishaji wa kijinsia, kwani wavulana hawapimwi ubikira. Wasichana huwekwa chini ya shinikizo kubwa, wengine huishi kwa hofu ya kukataliwa au hata kushutumiwa bila kosa.

Katika baadhi ya nchi kama Burundi, kipimo hiki hutumiwa hata msichana anaporipoti kubakwa — kwanza huangaliwa kama alikuwa bikira, jambo linalozidi kumuumiza kiakili badala ya kumsaidia.

Huko Morocco, baadhi ya wasichana hutumia tembe linaloitwa capsule du sang lenye unga mwekundu. Tembe hilo huingizwa ukeni kabla ya tendo la ndoa, likitoa damu bandia ili ionekane kuwa msichana alikuwa bikira. Hii hufanyika ili kuepuka aibu, kukataliwa na familia au kurudishwa nyumbani siku ya harusi.

Msichana mmoja alisema: “Si ni damu wanataka? Basi tunawapa damu.”

Desturi ya kupima ubikira inatokana na imani potofu kwamba ubikira ni hazina ya thamani kwa msichana. Hata hivyo, watetezi wa haki za wanawake wanasema ni utamaduni wa kunyanyasa na kuwadhalilisha wasichana.

Kwa sasa, mataifa mengi yanapaza sauti kutaka utaratibu huu ukomeshwe kabisa, kwa kuwa unakiuka haki za binadamu.

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *