Mwanasiasa wa upinzani nchini Burundi, Agathon Rwasa, ametangaza kuwa uchaguzi unaotarajiwa nchini humo si uchaguzi halisi bali ni maigizo yaliyopangwa na chama tawala cha CNDD-FDD kinachoongozwa na Rais Evariste Ndayishimiye.
Alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari nchini Burundi, ambapo alitoa wito wa kuitishwa kwa mkutano wa kitaifa kulaani utawala wa Rais Ndayishimiye ambao aliutaja kuwa wa kiimla.
Rwasa alieleza kuwa uchaguzi wa wabunge na wa viongozi wa mikoa (za komine) unaokuja umeongeza mvutano wa kisiasa nchini humo kutokana na matatizo mbalimbali yaliyopo kama vile kupuuzwa kwa raia, ukandamizaji, na ukosefu wa nafasi ya kidemokrasia.
Aliendelea kusema kuwa uchaguzi huu unaofanyika ni kama tamthilia iliyopangwa na CNDD-FDD, akisema: “Huu si uchaguzi, ni maigizo tu.”
Aidha, alisema kuwa hata kampeni zilizofanyika kabla ya uchaguzi huo zilikuwa sehemu ya maigizo hayo, akisema: “Hata kampeni zao ni burudani tu ya CNDD-FDD. Kila kitu kinaonekana kama kimekwisha pangwa.”
Rwasa alilishutumu chama tawala kwa kupenyeza itikadi zake katika taasisi zote zinazohusiana na uchaguzi, kuanzia ngazi za chini hadi tume ya uchaguzi, na kusema kuwa hii ni sababu nyingine inayoharibu uhalali wa uchaguzi huo.
Aliendelea kusisitiza kuwa kampeni zimefanyika katika hali ya woga, ambapo raia walitishwa na kundi la vijana wa Imbonerakure kutoka chama cha Evariste Ndayishimiye.
Mwisho alikemea matendo ya wale wanaohusishwa na serikali waliowanyang’anya raia baadhi kadi za kupigia kura na kuwatishia watu katika maeneo mbalimbali, hasa vijijini.


