Mwendesha mashtaka wa kijeshi mjini Kinshasa amewakamata wafanyabiashara watano (5) raia wa India na kufunga ghala lao lililoko Limeté, katikati ya mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya kugunduliwa kwa hifadhi kubwa ya mavazi ya kijeshi bandia, kama ilivyotangazwa Jumamosi, Mei 31, 2025.
Hasa katika Kinshasa na DRC kwa ujumla, sare hizi bandia za kijeshi zinajulikana kwa jina la “Zonkion”, lililotumiwa na msanii wa Kongo, Papa Wemba, aliyefariki huko Abidjan, Ivory Coast.
Mavazi haya pia yalijulikana sana katika kundi la muziki la Wenge Musica, yakijulikana kama “Pentagone”.
Kwa mujibu wa taarifa zilizofikia Shirika la Habari la Congo (ACP), ugunduzi wa kwanza ulifanyika katika ghala moja barabara ya 8, katika eneo la Limeté, ambapo mafungu 20 ya mavazi ya kijeshi bandia yalinaswa na waendesha mashtaka wa kijeshi.

Ugunduzi wa pili ulifanyika Ijumaa, ambapo mafungu mengine 85 ya mavazi hayo yalipatikana katika ghala hilo hilo barabara ya 8.
Katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, mkuu wa eneo la Limeté alitembelea eneo hilo na kuthibitisha kuwa kulikuwa na hifadhi kubwa ya mavazi ya kijeshi.
Ripoti ya ndani ya jiji la Kinshasa, linaloongozwa na Gavana Daniel Bumba, imethibitisha kuwa mavazi yaliyokamatwa ni sare bandia za kijeshi zinazojulikana kama “Zonkion” na “Pentagone”, ambazo hazihusiani na jeshi la taifa japokuwa zinafanana kwa muonekano.
Ghala hilo sasa limefungwa rasmi na ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi, huku mafungu 31 ya mavazi hayo yakiifadhiwa katika ofisi ya manispaa ya Limeté.
Kutokana na sababu za kiusalama hasa ikizingatiwa vita inayoendelea mashariki mwa nchi, mamlaka zimepiga marufuku kuvaa sare hizi bandia nchini kote kwa lengo la “kuzuia waasi wanaopenya”.


