Rais Félix Antoine Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alimkabidhi maua Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Thérèse Wagner Kayikwamba, kama ishara ya shukrani.
Tshisekedi alimshtua Kayikwamba wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika ofisini kwake.
Katika mkutano huo, Rais wa DRC alisifu kile alichokiita maendeleo makubwa ambayo nchi yake imepiga katika uwanja wa diplomasia ya kimataifa, “hasa katika suala la ukosefu wa usalama mashariki mwa nchi pamoja na mashambulizi ya kidiplomasia yaliyofanywa kupambana na uvamizi wa Rwanda.”
Aliongeza: “Maelekezo yalitolewa, na matokeo yanaonekana,” kabla ya kumtaja Kayikwamba kama “shujaa wa kweli.”
Tshisekedi alimkabidhi Waziri wake wa Mambo ya Nje maua, baada ya muda Kayikwamba akizunguka duniani kote akiomba mataifa kuchukua hatua dhidi ya Rwanda, kutokana na madai ya Kinshasa kuwa Rwanda inaunga mkono waasi wa M23.
Madai haya yameungwa mkono na nchi nyingi hasa za Magharibi, ambapo baadhi yao zimechukua hatua dhidi ya Rwanda na kulishinikiza “kuacha kuisaidia M23 na kuondoa majeshi yake kutoka ardhi ya DRC.”
Rwanda mara nyingi imelaumu msimamo wa nchi hizo kuwa wa upendeleo, zikilaumiwa kwa kuchukua upande mmoja badala ya kushughulikia chanzo halisi cha migogoro mashariki mwa DRC.
Kwa sasa, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa katika mazungumzo ya kupunguza mvutano kati ya nchi hizo mbili. Zinatarajiwa kusaini mkataba wa amani katika siku chache zijazo kwa msaada wa upatanisho kutoka Marekani.


