Viongozi wa Seneti ya Rwanda na Seneti ya Burundi walifanya mazungumzo siku ya Ijumaa, tarehe 20 Juni, kuhusu uhusiano wa mataifa yao ambao umekuwa wa wasiwasi kwa muda mrefu.
Mazungumzo hayo yalihusisha Rais wa Seneti ya Burundi, Mheshimiwa Emmanuel Sinzohagera, aliyekuwa ziarani nchini Rwanda, na mwenzake wa Rwanda, Dkt. François Xavier Kalinda, Rais wa Seneti ya Rwanda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Seneti ya Burundi katika mtandao wa X, viongozi hao walijadili nafasi ya taasisi zao katika kuimarisha uhusiano kati ya Burundi na Rwanda.
Ujumbe huo ulisema:
“Rais wa Seneti Mheshimiwa Sinzohagera Emmanuel asubuhi hii alikutana na mwenzake wa Rwanda akiwa na manaibu wake wote wawili katika ziara rasmi. Mazungumzo yao yalijikita kwenye jukumu la mabaraza haya mawili ya juu katika kuimarisha uhusiano kati ya Burundi na Rwanda.”
Kwa upande wake, Seneti ya Rwanda iliongeza kuwa marais hao walijadili pia kuhusu ushirikiano wa mabunge kupitia diplomasia ya kibunge.
Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi ulianza kuzorota mwishoni mwa mwaka 2023, na mapema mwaka 2024, Burundi ilifunga mipaka yake na Rwanda.
Gitega ilichukua hatua hiyo kwa madai kwamba Kigali inatoa msaada kwa kundi la waasi la RED-Tabara, linalopinga serikali ya Burundi—mashitaka ambayo serikali ya Rwanda imeyakanusha vikali mara nyingi.
Burundi pia imekuwa ikilituhumu Rwanda kwa kuwapokea watu wanaoshukiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya mwaka 2015 dhidi ya Rais wa zamani Pierre Nkurunziza, na imesisitiza mara kwa mara kwamba uhusiano haitaweza kurejea katika hali ya kawaida iwapo watu hao hawatakabidhiwa.
Mkutano wa marais wa Seneti wa mataifa haya mawili umefanyika wakati ambapo, miezi michache iliyopita, Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi alitoa vitisho vya kuingia vitani na Rwanda.
Aliituhumu Rwanda kwa kupanga kuivamia Burundi kupitia RED-Tabara, kwa mtindo unaofanana na ule wa kusaidia kundi la M23 linalopigana na jeshi la serikali ya DRC, ambalo linajumuisha pia wanajeshi wa Burundi.
Ingawa viongozi wa kidiplomasia kutoka pande zote mbili wamekutana mara kwa mara ili kupunguza mivutano, hakujapatikana suluhisho la moja kwa moja hadi sasa.


