Luteni Jenerali Jean Claude Kabeya, ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa karibu wa Rais Félix Tshisekedi tangu alipoingia madarakani mwaka 2019, amekamatwa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC).
Taarifa kutoka Kinshasa zinasema kuwa Lut. Jen. Kabeya alikamatwa na vyombo vya usalama asubuhi ya Jumatatu, tarehe 16 Juni 2025, ingawa sababu za kukamatwa kwake hazijatangazwa.
Kukamatwa kwake kunakuja huku kitengo cha ujasusi wa kijeshi cha DRC (DEMIAP) kikiwa kimewakamata maafisa wa ngazi za juu kwa siku kadhaa, bila kufichua mashitaka yao.
Kulingana na ripoti ya mashirika ya kiraia iliyotolewa hivi karibuni, kati ya waliokamatwa wapo majenerali wapatao 29.
Mashirika hayo yameitaka serikali kutowashikilia wanajeshi hao kwa muda mrefu bila kesi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Akijibu, msemaji wa jeshi la Congo, Jenerali Sylvain Ekenge, alisema kwamba “wakati wa vita, si lazima mchakato wa haraka wa kisheria ufuatwe kwa waliokamatwa.”
Wakati huo huo, wachambuzi wengi wa siasa wanaamini kwamba kukamatwa kwa maafisa hawa waandamizi kunahusiana na mvutano unaoongezeka kati ya serikali ya Congo na Rais wa zamani Joseph Kabila, ambaye hivi karibuni aliwasili Goma—eneo linalodhibitiwa na muungano wa AFC/M23 unaopinga serikali ya Kinshasa.
Lut. Jen. Kabeya aliteuliwa mwaka 2019 mara baada ya Tshisekedi kuingia madarakani, kuwa mkuu wa ofisi ya kijeshi iitwayo “Maison Militaire.”
Mwaka wa 2023 aliondolewa kwenye wadhifa huo na nafasi yake kuchukuliwa na Jen. Franck Ntumba. Tangu wakati huo, kulienea madai kuwa aliondolewa kwa sababu Rais Tshisekedi alipoteza imani naye, na pia hakupangiwa tena jukumu lolote rasmi.


