Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda, Victoire Ingabire Umuhoza, kiongozi wa chama cha Dalfa-Umurinzi, amejitenga na wafuasi wa chama chake wanaoshutumiwa kwa kupanga njama ya kuangusha serikali ya Rwanda.
Mahakama Kuu ilikuwa imemwita Ingabire kufika kutoa maelezo katika kesi inayoendelea dhidi ya washitakiwa tisa.
Katika vikao vya awali, waendesha mashtaka walimtaja Ingabire mara kadhaa, wakidai kuwa alihusika kikamilifu katika kuandaa mafunzo ya kuipindua serikali bila kutumia silaha, ambayo washitakiwa wanadaiwa kushiriki. Hiyo ndiyo sababu ya kuitwa kwake mahakamani.
Alhamisi hii, Ingabire alifika mahakamani na kukiri kuwafahamu washitakiwa wote, lakini alisisitiza kuwa yeye binafsi wala chama chake hawakuhusika katika kuandaa mafunzo hayo.
Alisema kuwa chama chake hakihusiki na tuhuma hizo, kwani Dalfa-Umurinzi si chama kilichosajiliwa kihalali, na juhudi zake zote za kukisajili hazikufanikiwa.
Akasema:
“Chama hicho hakiwezi kufanya chochote kwa kuwa hakitambuliki kisheria.”
Ingabire pia aliieleza mahakama kuwa baada ya kuona ugumu wa kukisajili chama hicho, aliagiza kamati ya muda aliyoiunda kusitisha shughuli zote, ikiwa ni pamoja na kutafuta wanachama.
Waendesha mashtaka wamehusisha mafunzo hayo na tukio la kila mwaka lijulikanalo kama “Ingabire Day”, linaloadhimishwa na baadhi ya Wanyarwanda waishio ughaibuni wanaomuunga mkono.
Mahakamani leo, Ingabire alifafanua kuwa mafunzo hayo hayana uhusiano wowote na siku ya “Ingabire Day”, akieleza kuwa tukio hilo huandaliwa na Wanyarwanda wa nje ya nchi, na kwamba yeye hashiriki katika mipango yake, ingawa wakati mwingine huombwa kutuma ujumbe.
Baada ya kumsikiliza, majaji walisema watajifungia kwa faragha kufanya tathmini kama maelezo aliyotoa yanatosha kabla ya kutoa uamuzi.


